Headlines News :
KARIBU ZANZIBAR YETU BLOG, KWA HABARI MOTO MOTO KUTOKA JIKONI USIKOSE KUTUFUATILIA...ZANZIBAR MEDIA GROUP TUNAIWAKILISHA ZANZIBAR...
Home » » Jamii yaaswa kutowadharau yatima

Jamii yaaswa kutowadharau yatima


Na Mwandishi wetu
JAMII imeaswa kuondokana na utamaduni wa kuwapeleka mayatima katika vituo vya kulelea watoto na badala yake  kuwalea katika familia, kwani hatua hiyo inazidisha upendo kwao.

Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Hifadhi ya mtoto, katika Idara ya Ustawi wa Jamii, Maria Obel Malila, wakati akitoa ufafanuzi katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi na walezi wa vituo vya kulelea watoto nchini, yaliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mafunzo Kilimani.

Alisema wananchi walio wengi wamejenga mazoea kuwa vituo vya kulelea watoto ndio mahala panapofaa zaidi kuwapeleka watoto yatima, ilhali kuna watu wa karibu wa kuwalea na kuwatunza vyema.

Alisema pale mtoto anapolelewa katika familia hupata upendo na kujengewa mazingira bora katika maisha yake ya baadae.

“Kumpeleka  mtoto kituoni iwe jambo la mwisho, pale ambapo hakuna jinsi, ni vyema watoto wakalelewa katika familia, hupata upendo na kujengewa mazingira bora ya maisha ya baadae,” alisema.

Aidha aliwataka baadhi ya watu wenye hulka ya kutafuta nafasi na kuwapeleka watoto wao kulelewa katika vituo vya kulelea watoto kwa kisingizio cha kuwa na uwezo wa duni kimaisha, kuondokana na tabia hiyo, kwani kimsingi watoto wanaopsawa kulelewa katika vituo hivyo ni yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu.

Katika hatua nyingine mwezeshaji Seif Maabad, akizungumzia mahitaji ya msingi ya mpango wa malezi ya kambo, alisema ni muhimu utafiti wa kina kufanyika kabla mlezi anaeomba  mtoto, kupatiwa mtoto huyo kwa ajili ya kwenda kuishi nae.

Alisema hatua hiyo ni muhimu, kwa vile itaiwezezesha Idara ya ustawi wa Jamii, kufahamu iwapo walezi  wanaomba mtoto  hawana kumbu kumbu za makosa ya udhalilishaji pamoja na kuwa na uwezo wa kumtunza vyema mtoto huyo.

Alisema baada ya mtoto kupelekewa katika malezi ya kambo, kuna umuhimu wa kufuatilia maendeleo na hali ya afya ya mtoto, elimu pamoja na ukuaji wake kisaikolojia katika jamii.

“Idara ya Ustawi wa jamii ina jukumu la kuwakabidhi watoto kwa walezi wa kambo, lakini pia kuwaongoza watoto katika kuangalia ustawi wao,” alisema.

Alitaka kuwepo mawasiliano ya kutosha kati ya walezi  wa mtoto na idara, kwa kuelewa kuwa afikapo umri wa miaka 18,mtoto  hulazimu kurejeshwa alikotoka.

Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoandaliwa na Idara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar na kufadhiliwa na UNICEF, yaliwashirikisha viongozi na walezi wa vituo kadhaa vya kulelea watoto ikiwemo SOS, Islah Centre,Saifo orphan Children,kituo cha kulelea watoto Mazizini,Fissabillillah Fuoni, Reema Home, Montessory Orphan Organisation,Wakfu Al Mazrui na Omar Al Khatab.
Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : Zanzibar Media Group
Copyright © 2020. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved