Headlines News :
KARIBU ZANZIBAR YETU BLOG, KWA HABARI MOTO MOTO KUTOKA JIKONI USIKOSE KUTUFUATILIA...ZANZIBAR MEDIA GROUP TUNAIWAKILISHA ZANZIBAR...
Home » » Zifahamu mbinu mbali mbali za uuzaji wa bangi

Zifahamu mbinu mbali mbali za uuzaji wa bangi

Na Juma Khamis

KILIO kikubwa bado kinaendelea kusikika kutoka kwa jamii ya wakazi wa Mji Mkongwe, juu ya tatizo la matumizi ya dawa za kulevya. Licha ya juhudi zinazochukuliwa na polisi, mahakama na watu binafsi, bado kundi kubwa la vijana katika mji huu wa kihistoria, wanaendelea kutumia dawa za kulevya; kuanzia bangi, mirungi, heroine na cocaine. 
Dawa hizi huvutwa katika chochoro za mji huu, kwenye majengo mabovu yaliyohamwa na kwenye fukwe. Baadhi ya nyumba ndio zinazotumika kuuza dawa hizi ingawa kwa siri sana kukwepa kukamatwa na polisi. 
Mara nyingi wauzaji hutumia matundu madogo yaliyowekwa kwenye madirisha; ambapo mnunuzi hutakiwa kupenyeza pesa kwanza ndipo apenyezewe dawa yake iliyofungwa kwenye karatasi ndogo.
Matumizi ya heroine na bangi yamechukua nafasi kubwa katika mji huu na ingawa idadi ya watumiaji inaendelea kupungua, lakini bado kuna vijana wenye umri wa kuanzia miaka 14-25 wanaochipukia kuvuta bangi. Mbali ya kuvuta, uchunguzi wa makala hii umegundua kuna biashara ya siri ya uuzaji wa bangi  iliyotengenezwa kama kashata. 
Kashata hii iliyotengenezwa kwa njugu, sukari, unga na hiliki pia imewekewa chembechembe za bangi na wateja wanajulikana; sio kila mtu anaweza kuuziwa. 
Baada ya kupewa taarifa, nilikwenda hadi eneo nililofahamishwa kuwa ndipo biashara hii inapofanyika, lakini juhudi zangu za kutaka kununua kuthibitisha ukweli wa taarifa hizi zilishindikana baada ya kukataliwa kuuziwa kwa madai tayari zilikuwa na wateja.
Lakini naambiwa biashara hii ilikuwa maarufu katika miaka ya 1990, kabla ya polisi kubaini biashara hiyo na kuanza kufuatilia. 
Mmoja ya wakazi wa mji huu unaovutia idadi kubwa ya watalii na uliosheheni biashara ya vinyago, Fatma Said (49), anasema kashata zilizochanganywa na unga wa bangi, zilikuwa zikipatikana zaidi katika miaka ya nyuma, lakini zilikuwa zikiuzwa kwa siri sana na wateja wote wanajulikana. 
Anasema kashata hizo zilikuwa haziuzwi hadharani lakini wateja wake walikuwa wengi, wengine wakitoka nje ya mji huo. ‘Kashata ya bangi si biashara ngeni hapa; kama hivi sasa wapo wanaouza watakuwa wachache sana, lakini miaka ya nyuma ilikuwa kazi maarufu, lakini hauziwi kila mtu,’ anasema. 
Mzee Ismail Seif (55), anakiri kwamba kashata zilizokuwa zimechangazwa na unga wa bangi, zilikuwa zinapatikana, lakini sasa wauzaji wamepungua sana kwa sababu polisi wamegundua mbinu hii. 
“Naamini hakuna tena wauzaji wa kashata ya bangi, lakini  enzi za ujana wetu watu walikuwa wakifanya biashara hii na ilikuwa na wateja,” anasema. 
Mohammed (majina yake mengine yamehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 35, mbali ya kukiri kuwa Mji Mkongwe kuwa kivutio cha watumiaji wengi wa dawa za kulevya, anasema alishawahi kula kashata iliyochanganywa na bangi katika kipindi chake cha kwanza cha kutumia dawa za kulevya.
“Kama hujaambiwa si rahisi kujua, mimi nilikuwa nauziwa kwa sababu nilikuwa mteja, lakini siku nyengine nilipokuwa nafuatana na rafiki zangu nilikuwa siuziwi, naambia zimeisha,”anasimulia. 
Sheha wa Shehia ya Mkuzani, Juma Mugheiry, mbali ya kuainisha mikakati wanayochukua kukabiliana na wimbi la matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo kuwatumia askari jamii, anasema bado tatizo lipo ingawa sio kubwa.
“Matumizi ya dawa za kulevya yamepungua, lakini tunao vijana bado wanaendelea kwa sababu dawa za kulevya zinapatikana humu mitaani mwetu,” alisema.
Mugheiry anasema baadhi ya vijana wanaendelea kutumia  bangi na heroine na kusababisha hofu kwa wenyeji na wageni wanaotembelea mji huo. 
Kuhusu kashata iliyochanganywa na unga wa bangi, anasema biashara hiyo ilikuwepo miaka ya nyuma lakini kwa sasa imepungua au haifanyiki tena. 
‘Ilikuwa ikifanyika, lakini baada ya polisi kugundua na kuanza kufuatilia, aidha itakuwa haifanyiki tena na kama inafanyika itakuwa kwa siri kubwa,’ anasema. 
Shauku yangu ya kutaka kufahamu ukweli wa biashara hii inanifanya nifunge safari hadi ofisi za Kitengo cha Kukabiliana na Dawa za Kulevya Zanzibar kilichopo chini ya Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, nyuma ya skuli ya msingi Jang’ombe. 
Hapa nakutana na Kaimu Mkuu wa kitengo hicho, Msaidizi Mkaguzi wa Polisi, Mngwali Ussi pamoja na Staff Sajenti, Mussa Hassan. Swali langu la kwanza kutaka kujua ni kama walishawahi kupata taarifa kuhusu kashata zilizochanganywa na unga wa bangi. 
Kabla ya kujibu swali langu hilo, Staff Sajenti Mussa Hassan, anasema bangi inaweza kusarifiwa kiasi ambacho kama askari hana utaalamu wa kufahamu, anaweza asiifahamu. 
Anasema kuna bangi ya kusindika (charas) ambayo haina tofauti na kipande cha sabuni au vinoo vinavyotumiwa na mafundi seremala na kamwe si rahisi kwa askari wa kawaida asie na elimu ya dawa za kulevya kufahamu. 
“Inawezekana baadhi ya askari wasio wa kitengo ambao wanafanya kazi ya kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya hawaifahamu bangi ya kusindika na inapita chini ya mikono yao,” anasema. 
Anasema kipande kimoja cha bangi ya kusindika kinaweza kuwa na uzito wa hadi kilo nne. 
Kuhusu kashata, Staff Sajenti Mussa, akizungumza kwa niaba ya DCI, Mussa Msangi, anasema ni kweli Mji Mkongwe kulikuwa na kashata zilizokuwa zikitengenezwa kwa unga wa bangi. 
“Kashata hizi zilikuwa na wateja wengi, kipindi fulani sisi tulikwenda kutaka kununua kuweka kama sampuli, kwa kweli wanachama wa kashata hii wanajulikana sio mtu yeyote anaweza kuuziwa,” anasema.
“Lakini tunaamini kashata hizi haziuzwi tena na kama zinauzwa ni kwa siri kubwa na ni vigumu kuwakamata wahusika kwa sababu kashata ni chakula cha kawaida,”anasema.
Hata hivyo, anashauri jamii kutoa ushirikiano katika mapambano dhidi ya biashara nzima ya dawa za kulevya, badala ya kuwaachia askari peke yao. 
‘Tunashindwa kwenye kesi zetu nyingi kwa sababu ya kukosekana mashahidi raia; sasa ili tushinde vita hivi lazima wananchi washiriki mapambano kwa kutoa ushahidi mahakamani kwa sababu kesi inapokosa shahidi raia, inakosa uzito na ni rahisi mshitakiwa kuachiwa kwa sababu siku zote mahakama inaona sisi askari tunakandamiza haki za raia,’ anasema. 
“Kazi yetu ni ngumu na kama wananchi wataendelea kuwalinda, ni vigumu kushinda kwa sababu wauzaji ni majirani zetu, wanatupa pesa, wametuchimbia visima, hapa ndio penye ugumu wa kutajwa,”anasema.
 
 
 
 
 
 
Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : Zanzibar Media Group
Copyright © 2020. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved