Headlines News :
KARIBU ZANZIBAR YETU BLOG, KWA HABARI MOTO MOTO KUTOKA JIKONI USIKOSE KUTUFUATILIA...ZANZIBAR MEDIA GROUP TUNAIWAKILISHA ZANZIBAR...
Home » , » Kesi za dawa za kulevya:Polisi, Mahakama, Mkemia, DPP watupiana mpira

Kesi za dawa za kulevya:Polisi, Mahakama, Mkemia, DPP watupiana mpira

Na Juma Khamis
INGAWA sheria ya kukabiliana na dawa za kulevya namba 9 ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011, inatoa adhabu kali kwa watumiaji, wasafirishaji na wamiliki wa dawa za kulevya, bado kuna manung’uniko mengi kuhusu jinsi kesi za dawa za kulevya zinavyoshughulikiwa.
Polisi ambao ndio wakamataji na wapelelezi pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ambao ndio wanaoshtaki, wanailaumu mahakama kwa jinsi inavyowaachia washtakiwa wa dawa za kulevya, huku mahakama nayo ikizitupia lawama taasisi hizo mbili kwa kushindwa kufanya upelelezi wa kina na kuthibitisha makosa dhidi ya washtakiwa.
Taasisi nyengine inayolaumiwa ni Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kufanya uchambuzi wa vielelezo vya dawa za kulevya.
Taasisi hii inadaiwa kuchelewesha kutoa matokeo ya uchambuzi na pale wanapotakiwa kufika mahakamani kutoa ushahidi wa kitaalamu, huwa wanakwepa.
Ili kuthibitisha madai hayo, mwandishi wa makala hii analazimika kuzifuata taasisi hizi ili kutaka kujua ukweli kuhusu kesi za dawa za kulevya.

Polisi
Naibu Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Zanzibar (DCI), Salum Msangi, anasema bado kuna tatizo kubwa katika kushughulikia kesi za washtakiwa wa dawa za kulevya.
Anasema  polisi wanajitahidi kukamata watuhumiwa wa dawa za kulevya na kuwashitaki, lakini baada ya kufika mahakamani huachiwa ama kwa dhamana katika kipindi kifupi na kusababisha kuruka dhamana na mara nyingi kesi za washtakiwa wa dawa za kulevya hufutwa kabisa kwa madai ya kukosekana ushahidi.
Aidha anasema kesi  za dawa za kulevya huchukua muda mrefu sana kumalizika kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kuchelewa majibu ya vielelezo kutoka kwa Mkemia.
Anasema kitendo cha mahakama kuchelewesha kesi sana, kunawafanya mashahidi raia kugoma kufika mahakamani kutoa ushahidi, lakini mara nyengine hutishiwa na wenye kesi na kuhongwa kiasi kikubwa cha fedha ili wasiende kutoa ushahidi.
Pia anasema kuna hisia kwamba vielelezo vya dawa za kulevya vinarejea tena mitaani kwa sababu hakuna mfumo mzuri wa kuharibu.

Staff Sajenti Hassan Mussa, anasema kuna ucheleweshaji mkubwa wa vielelezo kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu ambapo kielelezo kimoja kinaweza kuchukua hadi wiki mbili hakijaandikiwa ripoti ingawa uchunguzi unakuwa umeshakamilika.
“Tunakwenda na vielelezo tunazungushwa hadi wiki mbili mpaka tatu hatujapata ripoti, hali hii inatuvunja moyo na inasababisha tushindwe katika kesi zetu,  kuna wakati mwengine vielelezo vinapotea huko huko,”anasema.

Ofisi ya Mkemia
Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeanzishwa kwa sheria namba 10 ya mwaka 2011, ambapo pamoja na majukumu mengini ya msingi inawajibu wa kuchunguza kemikali zikiwemo dawa za kulevya.
Mchambuzi wa chakula na dawa, Maryam Amour Hamad, akizungumza kwa niaba ya  Mkemia Mkuu, Dk. Islim Juma, anasema pamoja na kukabiliwa na uchache wa vifaa vya maabara, uchunguzi wa dawa za kulevya unafanyika kwa wakati, lakini polisi wenyewe ndio wanaochelewa kuchukua ripoti za uchunguzi.
“Tuna wataalamu wa kutosha, haichukuwi hata saa mbili tumeshamaliza kufanya uchunguzi na baadae kuandika ripoti, lakini wanaoleta vielelezo ndio wanaochelewa kuja kuchukua,” anasema.
Kuhusu madai kwamba maofisa wa ofisi hiyo wanashindwa kufika mahakamani kutoa ushahidi, anasema  inatokana na upungufu wa wachunguzi wa vielelezo, ambapo kwa sasa wako wawili tu ndio wenye sifa ya kutoa ushahidi mahakamani.
“Mara nyingi sisi ndio tunaotupiwa lawama ya kuchelewesha ripoti, lakini polisi wao hawafanyi kazi zao vizuri; wanachelewa kuja kuchukua ripoti za uchunguzi,”anasema.
Mkurugenzi wa Mashtaka
Mkurugenzi wa Mashtaka, Ibrahim Mzee Ibrahim,  akizungumza ofisini kwake uwanja wa Tumbaku, anasema taasisi zinazoshughulikia vielelezo vya dawa za kulevya haziko makini, kwani vielelezo vinaweza kukaa hadi siku nne kabla ya kufanyiwa kazi.
Lakini pia anasema polisi wanachelewesha kesi; wanachukua muda mrefu sana tangu watuhumiwa wakamatwe, vielelezo (dawa) kupelekwa kwa Mkemia kuchunguza na kufanya upelelezi.
“Tunashindwa kwenye kesi za dawa za kulevya kwa sababu ya kukatisha  mfumo mzima wa kushughulikia kesi za aina hii; kitendo cha dawa za kulevya  kubakia polisi hadi  ushahidi uanze kutolewa, kunatoa mwanya ushahidi kupotea,”anasema.
“Usafirishaji wa dawa za kulevya ni kosa ambalo kwa kawaida  mtuhumiwa hapewi dhamana, lakini ni tofauti hapa kwetu, mara nyingi mahakama zimekuwa zikikataa ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusu usafirishaji na badala yake wanasema mshitakiwa alikuwa anamiliki ili kutoa mwanya wa kumpa dhamana,’ anasema.
“Kuna mshitakiwa mmoja alifika uwanja wa ndege akiwa kwenye teksi, ana pasipoti, tiketi ya ndege na viza yake pamoja na begi lenye dawa za kulevya. Akashuka kwenye teksi akaenda kufanya ukaguzi, baada ya kumaliza ukaguzi akakamatwa, lakini baada ya kumfikisha mahakamani, hakimu alisema alikuwa hasafirishi badala yake anamiliki, kwa hivyo akapewa dhamana na hadi sasa hajulikani alipo,”alisema.
Ibrahim anasema hali hii inasababisha ofisi yake kutokuwa na kesi nyingi za wasafirishaji na wamiliki wa dawa za kulevya, badala yake wana mzigo wa kesi za watumiaji.
Mahakama
Mrajisi wa Mahakama Kuu Zanzibar, George Kazi, anakiri kwamba kesi za dawa za kulevya zina changamoto kubwa; lakini mahakama inatekeleza wajibu wake wa kutoa haki sawa kwa pande zote.
Kesi za dawa za kulevya
Licha ya polisi kuendelea kuwakamata watu wanaosafirisha na kumiliki dawa za kulevya, bado kesi nyingi zinaendelea kukwama mahakamani na nyingi zimekuwa zikifutwa kwa kukosekana ushahidi.
Kwa mfano kuanzisha Januari hadi Disemba 2014, kitengo cha kukabiliana na dawa za kulevya kilikamata kesi 80 za usafirishaji na umiliki wa dawa za kulevya zenye washtakiwa zaidi ya 120, lakini ni kesi 8 tu kubwa zilizofunguliwa mahakamani, moja imefutwa na saba zinaendelea.
Aidha mwaka 2003, kesi 11 kubwa za usafirishaji na umiliki zilifunguliwa, kesi sita zimefutwa na tano tu zinaendelea.
Mwaka 2012 kulikuwa na kesi 26 zilizofunguliwa, kesi 17 zilifutwa, tano zinaendelea na mbili tu ndizo washtakiwa wanatumikia vifungo vya miaka saba na 15 jela, ingawa wamekata rufaa mahakama kuu.
Kwa ujumla, kuanzia 2012 -2014 ni kesi mbili tu ndizo zilizopata hukumu ya vifungo vya muda mrefu.
Jedwali la kesi za dawa za kulevya zilizokamatwa 2014
Aina ya dawa      
Zilizo mahakamani     
Zilizofutwa     
Zinazopelelezwa
Cocaine- 3
2
-
1
Heroine-53
45
1
7
Bangi-22
19
1
2
Vallium -2
2
-
-
Chanzo: Kitengo cha Kukabiliana na Dawa za Kulevya cha Polisi
Jadweli la kesi za dawa za kulevya mahakamani Vuga-Heroine, Cocaine 2012-2014
Mwaka
Kesi zilizofunguliwa
Zilizotolewa uamuzi
Zinazoendelea
2012
26
21 kesi zote
4-zilitiwa hatiani
1-faini 500,000/-kifungo mwaka mmoja
1-faini 700,000/-
1-kifungo miaka 7
1-kifungo miaka 15 na faini 4,000,000/-
17-zimefutwa
5
2013
11
6-kesi zote
-Zote sita zimefutwa
5
2014
8
1-imefutwa
7
Chanzo: Mahakama Vuga

Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : Zanzibar Media Group
Copyright © 2020. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved