Headlines News :
KARIBU ZANZIBAR YETU BLOG, KWA HABARI MOTO MOTO KUTOKA JIKONI USIKOSE KUTUFUATILIA...ZANZIBAR MEDIA GROUP TUNAIWAKILISHA ZANZIBAR...
Home » , » Changamoto za kiuchumi zinavyoutafuna msitu Jozani

Changamoto za kiuchumi zinavyoutafuna msitu Jozani

NA JUMA JUMA

 Zanzibar kama zilivyo nchi nyengine za Afrika, inashuhudia mageuzi ya haraka ya kiuchumi na kijamii ambayo yana mchango mkubwa katika uharibifu wa misitu. Ongezeko la watu, uwekezaji katika sekta ya utalii, vikundi vya kuweka na kukopa na ujenzi wa miundombinu, kumeakisi mabadaliko ya wazi kwa rasilimali ya misitu. Sensa ya watu na makazi ya 2012, inaonesha Zanzibar kuna wakazi 1.3 milioni kiwango ambacho ni ukuaji wa asilimia 2.8 kwa mwaka. Magezui haya yanatoa shinikizo kubwa si kwa misitu tu lakini hata wanyama kama kima punju (mbega mwekundu), ambae anapatikana Zanzibar pekee.



Mnyama huyu yuko hatarini na Shirika la Kuhifadhi Wanyama Duniani (IUCN) limemuweka kwenye mstari mwekundu. Kuanzia 2013-2015 hekta 65 za msitu wa Jozani ziliharibiwa na kusababisha hasara ya zaidi ya sh.4 bilioni na baadhi ya viumbe adimu kufa. Uharibifu huu umesababisha na uvunaji wa asali na ukataji magogo kwa uchomaji mkaa.

Kwa mujibu ya Sera ya Mazingira ya 2013, matumizi ya nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni asilimia 97. ATHARI ZA KIUCHUMI Kuongezeka shughuli za kiuchumi hasa vikundi vya kuweka na kukopa (saccos), kumeleta athari kwa misitu, ukiwemo Jozani. Ingawa mfumo huo unapata mafanikio, lakini umeiacha rasilimali ya misitu kwenye hatari kubwa.

 Mchumi Mohammed Fadhil, anasema mfumo wa kuweka akiba umebadili maisha ya kaya nyingi, ambapo wastani wa kipato cha mtu kimengozeka hadi kufikia zaidi ya dola 674 za Marekani. Pia kuna mafanikio katika kupunguza umaskini, ambapo wananchi wanaoishi chini ya kiwango cha mahitaji wamepungua kutoka asilimia 34.9 mwaka 2010 hadi asilimia 30.4 mwaka 2015.

 Anasema takwimu hizo pia zimechangiwa na kuwepo vikundi vya kuweka na kukopa vijijini, hata hivyo vinaleta tishio kwa maliasili kama misitu. “Wakazi wa vijijini hasa wanawake wamejiunga na saccos, lakini bado hawana mfumo mzuri wa kupata fedha za kuweka kwenye vikundi, hivyo wengi wanategemea misitu,” anasema. Kauli yake, inaungwa mkono na Naibu Katibu wa Jumuiya ya Hifadhi ya Mazingira Jozani (JECA), Awesu Shaaban.

 Anasema wanawake wengi wa vijijini hawana ajira rasmi hali hiyo inawafanya kurudi kwenye msitu kukata kuni ili wapate pesa za kuweka kwenye vikundi vyao. “Kuweka na kukopa ni mfumo mzuri, hata hivyo kupata fedha ni vigumu sana. Hii inatoa shinikizo kwa wanavijiji kufanya kila aina ya kazi ili wapate pesa ikiwemo kukata magogo kwa ajili ya kuni na mkaa,” anasema. "Uharibifu wa msitu ni wa kutisha.

 Utamuona mtu anajiunga na vikundi vitatu wakati hana kazi, sasa atapata wapi pesa za kuweka? Anachofanya ni kuingia msituni kukata kuni, tatizo hili ni hasa Jozani” anasema mwanakijiji wa Bwejuu, Abdala Mussa na kuongeza, “Watu hawana kazi na bila kuingia msituni kukata kuni na kuchoma mkaa hawawezi kupata pesa.” Mzigo mmoja wa kuni huuzwa sh. 3,000 hadi 5000 wakati kipolo kimoja cha mkaa wanauza hadi sh.10,000.

Mkurugenzi Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, Soud Mohammad Juma, anasema shughuli za kiuchumi zinaharibu msitu wa Jozani. “Wananchi ndio chanzo cha uharibifu huu, wengi hawafahamu umuhimu wa misitu, wanachoangalia ni vipi watapata fedha,” anasema. Anasema ingawa wanajitahidi kuulinda msitu, lakini kuna wimbi kubwa la uvunaji haramu wa mistu unaofanywa na wanavijiji. “Kuna kesi nyingi za watu waliokamatwa wakiharibu msitu, lakini hakuna hatua za maana zilizochukuliwa, hili linatuvunja moyo, lhata hivyo hatutachoka kuendelea kuwapa elimu,” anasema.

 Aidha anasema, rushwa muhali pia imechangia na ili kukabiliana na tatizo hilo, wamejaribu kubadilisha walinzi akiamini inaweza kusaidia kupunguza tatizo.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo, Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed, anasema ukataji miti kwa shughuli za kiuchumi unaendelea kuharibu uoto wa asili katika msitu wa Jozani. “Kama hatua za haraka hazitachukuliwa, katika kipindi kifupi kijacho msitu utatoweka kabisa na itabaki historia tu,” anasema. “Bekari zote za Zanzibar zinatumia nishati ya kuni kwa ajili ya kuchomea mikate, kuni hizi zinakatwa kwenye misitu, hivyo lazima tuwadhibiti,” anasema. UTALII Ongezeko la miradi ya utalii nalo inatoa tishio kwa rasilimali za misitu. Miradi hiyo mbali ya kuhitaji maeneo ardhi pia inahitaji miti hali ambayo imesababisha ‘majangili’ kuvamia misitu.

 Kwa mujibu wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, kuna hoteli na nyumba za kulaza wageni 329 na wastani wa watalii 350,000 wanatembelea kwa mwaka. Kati ya watalii wote, 50,000 wanakwenda Jozani kuangalia kima punju, ambapo kila mtalii analipia shilingi 20,000.

Hata hivyo, Waziri Hamad anasema, kutokana na kuongezeka uharibifu, idadi ya watalii inaweza kushuka kwa sababu kima ambao ndio kivutio wanakimbia kutokana na uharibifu.

 KIJAMII Msitu wa Jozani umesaidia kubadili maisha ya wanavijiji. Asilimia 80 ya fedha zote zinazokusanywa hapa zinatokana na kima ambapo nusu zinakwenda kwa wanavijiji.

 Kwa mwaka 2016, wanavijiji walilipwa sh.215.4 milioni Jumuiya nne zilifaidika na fedha ambazo ni Umoja wa Wenye Mashamba Jozani (UWEMAJO) iliyopata sh. 136.17 milioni, Kamati ya Hifadhi Pete sh. 28.67 milioni na Jumuiya ya Uhifadhi Mazingira Jozani (JECA), iliyopata sh. 12.3. milioni Waziri Hamad, anasema licha ya juhudi hizo bado wananchi hawajaacha kuharibu msitu.

Lakini Naibu Katibu wa Jumuiya ya Uhifadhi Mazingira Jozani (JECA), Awesu Shaaban, anasema mgao wanaopata wanavijiji unasaidia kwenye shughuli za maendeleo na sio kutatua shida za mtu mmoja mmoja. “Fedha zinasaidia kupunguza changamoto za maendeleo ya vijiji na si mtu mmoja mmoja hivyo tatizo la uharibifu msitu bado linaendelea kila siku,” anasema.

 Anasema kwa sababu wanavijiji bado wanahitaji kutumia misitu kwa hali yoyote, inasababisha baadhi ya walinzi kushambuliwa kutokana na kuingilia maslahi ya watu.

ELIMU WA UHIFADHI Waziri wa Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi, Hamad Rashid, asema serikali kwa kushirikiana na asasi za kiraia inatoa elimu ya uhifadhi wa msitu. Hata hivyo, bado uharibifu wa msitu ni wa kutisha. “Unakapopita nje utaona msitu uko timamu (uko vizuri) lakini ukiingia ndani utaona jinsi ulivyoharibiwa, hakuna kitu kilichobakia,” anasema.

SULUHISHO Waziri Hamad anasema ili kupunguza uharibifu, serikali inaendelea kutoa elimu kwa wanavijiji na kuwapatia mafunzo walinzi ili kuwa na uwezo wa kukabiliana na wahalifu. Mkurugenzi Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, Soud Mohammad Juma, anasema kuna haja kwa polisi na vyombo vya sheria kutoa adhabu kali kwa watu wanaokamatwa wakiharibu misitu kwani itakuwa funzo kwa wengine.
Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : Zanzibar Media Group
Copyright © 2020. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved