INGAWA
sheria ya kukabiliana na dawa za kulevya namba 9 ya mwaka 2009 kama
ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2011, inatoa adhabu kali kwa watumiaji,
wasafirishaji na wamiliki wa dawa za kulevya, bado kuna manung’uniko mengi
kuhusu jinsi kesi za dawa za kulevya zinavyoshughulikiwa.
Polisi
ambao ndio wakamataji na wapelelezi pamoja na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
ambao ndio wanaoshtaki, wanailaumu mahakama kwa jinsi inavyowaachia washtakiwa
wa dawa za kulevya, huku mahakama nayo ikizitupia lawama taasisi hizo mbili kwa
kushindwa kufanya upelelezi wa kina na kuthibitisha makosa dhidi ya washtakiwa.
Taasisi
nyengine inayolaumiwa ni Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ambayo ndiyo yenye
mamlaka ya kufanya uchambuzi wa vielelezo vya dawa za kulevya.
Taasisi
hii inadaiwa kuchelewesha kutoa matokeo ya uchambuzi na pale wanapotakiwa
kufika mahakamani kutoa ushahidi wa kitaalamu, huwa wanakwepa.
Ili
kuthibitisha madai hayo, mwandishi wa makala hii analazimika kuzifuata taasisi
hizi ili kutaka kujua ukweli kuhusu kesi za dawa za kulevya.
Polisi
Naibu
Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai Zanzibar (DCI), Salum Msangi,
anasema bado kuna tatizo kubwa katika kushughulikia kesi za washtakiwa wa dawa
za kulevya.
Anasema polisi wanajitahidi kukamata watuhumiwa wa
dawa za kulevya na kuwashitaki, lakini baada ya kufika mahakamani huachiwa ama
kwa dhamana katika kipindi kifupi na kusababisha kuruka dhamana na mara nyingi
kesi za washtakiwa wa dawa za kulevya hufutwa kabisa kwa madai ya kukosekana
ushahidi.
Aidha
anasema kesi za dawa za kulevya huchukua
muda mrefu sana kumalizika kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo kuchelewa
majibu ya vielelezo kutoka kwa Mkemia.
Anasema
kitendo cha mahakama kuchelewesha kesi sana, kunawafanya mashahidi raia kugoma
kufika mahakamani kutoa ushahidi, lakini mara nyengine hutishiwa na wenye kesi
na kuhongwa kiasi kikubwa cha fedha ili wasiende kutoa ushahidi.
Pia
anasema kuna hisia kwamba vielelezo vya dawa za kulevya vinarejea tena mitaani
kwa sababu hakuna mfumo mzuri wa kuharibu.
Staff
Sajenti Hassan Mussa, anasema kuna ucheleweshaji mkubwa wa vielelezo kutoka
Ofisi ya Mkemia Mkuu ambapo kielelezo kimoja kinaweza kuchukua hadi wiki mbili
hakijaandikiwa ripoti ingawa uchunguzi unakuwa umeshakamilika.
“Tunakwenda
na vielelezo tunazungushwa hadi wiki mbili mpaka tatu hatujapata ripoti, hali
hii inatuvunja moyo na inasababisha tushindwe katika kesi zetu, kuna wakati mwengine vielelezo vinapotea huko
huko,”anasema.
Ofisi ya Mkemia
Ofisi
ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeanzishwa kwa sheria namba 10 ya mwaka 2011,
ambapo pamoja na majukumu mengini ya msingi inawajibu wa kuchunguza kemikali
zikiwemo dawa za kulevya.
Mchambuzi
wa chakula na dawa, Maryam Amour Hamad, akizungumza kwa niaba ya Mkemia Mkuu, Dk. Islim Juma, anasema pamoja
na kukabiliwa na uchache wa vifaa vya maabara, uchunguzi wa dawa za kulevya
unafanyika kwa wakati, lakini polisi wenyewe ndio wanaochelewa kuchukua ripoti
za uchunguzi.
“Tuna
wataalamu wa kutosha, haichukuwi hata saa mbili tumeshamaliza kufanya uchunguzi
na baadae kuandika ripoti, lakini wanaoleta vielelezo ndio wanaochelewa kuja
kuchukua,” anasema.
Kuhusu
madai kwamba maofisa wa ofisi hiyo wanashindwa kufika mahakamani kutoa
ushahidi, anasema inatokana na upungufu
wa wachunguzi wa vielelezo, ambapo kwa sasa wako wawili tu ndio wenye sifa ya
kutoa ushahidi mahakamani.
“Mara
nyingi sisi ndio tunaotupiwa lawama ya kuchelewesha ripoti, lakini polisi wao
hawafanyi kazi zao vizuri; wanachelewa kuja kuchukua ripoti za uchunguzi,”anasema.
Mkurugenzi wa Mashtaka
Mkurugenzi
wa Mashtaka, Ibrahim Mzee Ibrahim,
akizungumza ofisini kwake uwanja wa Tumbaku, anasema taasisi
zinazoshughulikia vielelezo vya dawa za kulevya haziko makini, kwani vielelezo
vinaweza kukaa hadi siku nne kabla ya kufanyiwa kazi.
Lakini
pia anasema polisi wanachelewesha kesi; wanachukua muda mrefu sana tangu
watuhumiwa wakamatwe, vielelezo (dawa) kupelekwa kwa Mkemia kuchunguza na
kufanya upelelezi.
“Tunashindwa
kwenye kesi za dawa za kulevya kwa sababu ya kukatisha mfumo mzima wa kushughulikia kesi za aina
hii; kitendo cha dawa za kulevya kubakia
polisi hadi ushahidi uanze kutolewa,
kunatoa mwanya ushahidi kupotea,”anasema.
“Usafirishaji
wa dawa za kulevya ni kosa ambalo kwa kawaida
mtuhumiwa hapewi dhamana, lakini ni tofauti hapa kwetu, mara nyingi
mahakama zimekuwa zikikataa ushahidi wa upande wa mashtaka kuhusu usafirishaji
na badala yake wanasema mshitakiwa alikuwa anamiliki ili kutoa mwanya wa kumpa
dhamana,’ anasema.
“Kuna
mshitakiwa mmoja alifika uwanja wa ndege akiwa kwenye teksi, ana pasipoti,
tiketi ya ndege na viza yake pamoja na begi lenye dawa za kulevya. Akashuka
kwenye teksi akaenda kufanya ukaguzi, baada ya kumaliza ukaguzi akakamatwa,
lakini baada ya kumfikisha mahakamani, hakimu alisema alikuwa hasafirishi
badala yake anamiliki, kwa hivyo akapewa dhamana na hadi sasa hajulikani alipo,”alisema.
Ibrahim
anasema hali hii inasababisha ofisi yake kutokuwa na kesi nyingi za
wasafirishaji na wamiliki wa dawa za kulevya, badala yake wana mzigo wa kesi za
watumiaji.
Mahakama
Mrajisi
wa Mahakama Kuu Zanzibar, George Kazi, anakiri kwamba kesi za dawa za kulevya
zina changamoto kubwa; lakini mahakama inatekeleza wajibu wake wa kutoa haki
sawa kwa pande zote.
Kesi za dawa za kulevya
Licha
ya polisi kuendelea kuwakamata watu wanaosafirisha na kumiliki dawa za kulevya,
bado kesi nyingi zinaendelea kukwama mahakamani na nyingi zimekuwa zikifutwa
kwa kukosekana ushahidi.
Kwa
mfano kuanzisha Januari hadi Disemba 2014, kitengo cha kukabiliana na dawa za
kulevya kilikamata kesi 80 za usafirishaji na umiliki wa dawa za kulevya zenye
washtakiwa zaidi ya 120, lakini ni kesi 8 tu kubwa zilizofunguliwa mahakamani,
moja imefutwa na saba zinaendelea.
Aidha
mwaka 2003, kesi 11 kubwa za usafirishaji na umiliki zilifunguliwa, kesi sita
zimefutwa na tano tu zinaendelea.
Mwaka 2012 kulikuwa na kesi 26 zilizofunguliwa,
kesi 17 zilifutwa, tano zinaendelea na mbili tu ndizo washtakiwa wanatumikia
vifungo vya miaka saba na 15 jela, ingawa wamekata rufaa mahakama kuu.
Kwa ujumla, kuanzia 2012 -2014 ni kesi mbili tu
ndizo zilizopata hukumu ya vifungo vya muda mrefu.
Jedwali la kesi za dawa za kulevya zilizokamatwa 2014
Aina ya
dawa
|
Zilizo
mahakamani
|
Zilizofutwa
|
Zinazopelelezwa
|
Cocaine- 3
|
2
|
-
|
1
|
Heroine-53
|
45
|
1
|
7
|
Bangi-22
|
19
|
1
|
2
|
Vallium -2
|
2
|
-
|
-
|
Chanzo: Kitengo
cha Kukabiliana na Dawa za Kulevya cha Polisi
Jadweli
la kesi za dawa za kulevya mahakamani Vuga-Heroine, Cocaine 2012-2014
Mwaka
|
Kesi zilizofunguliwa
|
Zilizotolewa uamuzi
|
Zinazoendelea
|
2012
|
26
|
21 kesi zote
4-zilitiwa hatiani
1-faini 500,000/-kifungo mwaka mmoja
1-faini 700,000/-
1-kifungo miaka 7
1-kifungo miaka 15 na faini 4,000,000/-
17-zimefutwa
|
5
|
2013
|
11
|
6-kesi zote
-Zote sita zimefutwa
|
5
|
2014
|
8
|
1-imefutwa
|
7
|
Chanzo:
Mahakama Vuga
No comments:
Post a Comment