Na Juma Khamis
KILIO kikubwa bado kinaendelea kusikika kutoka kwa jamii ya wakazi wa Mji Mkongwe, juu ya tatizo la matumizi ya dawa za kulevya. Licha ya juhudi zinazochukuliwa na polisi, mahakama na watu binafsi, bado kundi kubwa la vijana katika mji huu wa kihistoria, wanaendelea kutumia dawa za kulevya; kuanzia bangi, mirungi, heroine na cocaine.
Dawa hizi huvutwa katika chochoro za mji huu,
kwenye majengo mabovu yaliyohamwa na kwenye fukwe. Baadhi ya nyumba ndio
zinazotumika kuuza dawa hizi ingawa kwa siri sana kukwepa kukamatwa na polisi.
Mara nyingi wauzaji hutumia matundu madogo
yaliyowekwa kwenye madirisha; ambapo mnunuzi hutakiwa kupenyeza pesa kwanza
ndipo apenyezewe dawa yake iliyofungwa kwenye karatasi ndogo.
Matumizi ya heroine na bangi yamechukua nafasi
kubwa katika mji huu na ingawa idadi ya watumiaji inaendelea kupungua, lakini
bado kuna vijana wenye umri wa kuanzia miaka 14-25 wanaochipukia kuvuta bangi. Mbali
ya kuvuta, uchunguzi wa makala hii umegundua kuna biashara ya siri ya uuzaji wa
bangi iliyotengenezwa kama kashata.
Kashata hii iliyotengenezwa kwa njugu, sukari,
unga na hiliki pia imewekewa chembechembe za bangi na wateja wanajulikana; sio
kila mtu anaweza kuuziwa.
Baada ya kupewa taarifa, nilikwenda hadi eneo
nililofahamishwa kuwa ndipo biashara hii inapofanyika, lakini juhudi zangu za
kutaka kununua kuthibitisha ukweli wa taarifa hizi zilishindikana baada ya
kukataliwa kuuziwa kwa madai tayari zilikuwa na wateja.
Lakini naambiwa biashara hii ilikuwa maarufu
katika miaka ya 1990, kabla ya polisi kubaini biashara hiyo na kuanza
kufuatilia.
Mmoja ya wakazi wa mji huu unaovutia idadi kubwa
ya watalii na uliosheheni biashara ya vinyago, Fatma Said (49), anasema kashata
zilizochanganywa na unga wa bangi, zilikuwa zikipatikana zaidi katika miaka ya
nyuma, lakini zilikuwa zikiuzwa kwa siri sana na wateja wote wanajulikana.
Anasema kashata hizo zilikuwa haziuzwi hadharani
lakini wateja wake walikuwa wengi, wengine wakitoka nje ya mji huo. ‘Kashata ya
bangi si biashara ngeni hapa; kama hivi sasa wapo wanaouza watakuwa wachache
sana, lakini miaka ya nyuma ilikuwa kazi maarufu, lakini hauziwi kila mtu,’
anasema.
Mzee Ismail Seif (55), anakiri kwamba kashata
zilizokuwa zimechangazwa na unga wa bangi, zilikuwa zinapatikana, lakini sasa
wauzaji wamepungua sana kwa sababu polisi wamegundua mbinu hii.
“Naamini hakuna tena wauzaji wa kashata ya
bangi, lakini enzi za ujana wetu watu
walikuwa wakifanya biashara hii na ilikuwa na wateja,” anasema.
Mohammed (majina yake mengine yamehifadhiwa)
mwenye umri wa miaka 35, mbali ya kukiri kuwa Mji Mkongwe kuwa kivutio cha
watumiaji wengi wa dawa za kulevya, anasema alishawahi kula kashata
iliyochanganywa na bangi katika kipindi chake cha kwanza cha kutumia dawa za
kulevya.
“Kama hujaambiwa si rahisi kujua, mimi nilikuwa
nauziwa kwa sababu nilikuwa mteja, lakini siku nyengine nilipokuwa nafuatana na
rafiki zangu nilikuwa siuziwi, naambia zimeisha,”anasimulia.
Sheha wa Shehia ya Mkuzani, Juma Mugheiry, mbali
ya kuainisha mikakati wanayochukua kukabiliana na wimbi la matumizi ya dawa za
kulevya ikiwemo kuwatumia askari jamii, anasema bado tatizo lipo ingawa sio
kubwa.
“Matumizi ya dawa za kulevya yamepungua, lakini
tunao vijana bado wanaendelea kwa sababu dawa za kulevya zinapatikana humu
mitaani mwetu,” alisema.
Mugheiry anasema baadhi ya vijana wanaendelea
kutumia bangi na heroine na kusababisha
hofu kwa wenyeji na wageni wanaotembelea mji huo.
Kuhusu kashata iliyochanganywa na unga wa bangi,
anasema biashara hiyo ilikuwepo miaka ya nyuma lakini kwa sasa imepungua au
haifanyiki tena.
‘Ilikuwa ikifanyika, lakini baada ya polisi
kugundua na kuanza kufuatilia, aidha itakuwa haifanyiki tena na kama inafanyika
itakuwa kwa siri kubwa,’ anasema.
Shauku yangu ya kutaka kufahamu ukweli wa
biashara hii inanifanya nifunge safari hadi ofisi za Kitengo cha Kukabiliana na
Dawa za Kulevya Zanzibar kilichopo chini ya Makao Makuu ya Polisi Zanzibar,
nyuma ya skuli ya msingi Jang’ombe.
Hapa nakutana na Kaimu Mkuu wa kitengo hicho,
Msaidizi Mkaguzi wa Polisi, Mngwali Ussi pamoja na Staff Sajenti, Mussa Hassan.
Swali langu la kwanza kutaka kujua ni kama walishawahi kupata taarifa kuhusu
kashata zilizochanganywa na unga wa bangi.
Kabla ya kujibu swali langu hilo, Staff Sajenti
Mussa Hassan, anasema bangi inaweza kusarifiwa kiasi ambacho kama askari hana
utaalamu wa kufahamu, anaweza asiifahamu.
Anasema kuna bangi ya kusindika (charas) ambayo
haina tofauti na kipande cha sabuni au vinoo vinavyotumiwa na mafundi seremala
na kamwe si rahisi kwa askari wa kawaida asie na elimu ya dawa za kulevya
kufahamu.
“Inawezekana baadhi ya askari wasio wa kitengo
ambao wanafanya kazi ya kukabiliana na uhalifu wa dawa za kulevya hawaifahamu
bangi ya kusindika na inapita chini ya mikono yao,” anasema.
Anasema kipande kimoja cha bangi ya kusindika
kinaweza kuwa na uzito wa hadi kilo nne.
Kuhusu kashata, Staff Sajenti Mussa, akizungumza
kwa niaba ya DCI, Mussa Msangi, anasema ni kweli Mji Mkongwe kulikuwa na
kashata zilizokuwa zikitengenezwa kwa unga wa bangi.
“Kashata hizi zilikuwa na wateja wengi, kipindi
fulani sisi tulikwenda kutaka kununua kuweka kama sampuli, kwa kweli wanachama
wa kashata hii wanajulikana sio mtu yeyote anaweza kuuziwa,” anasema.
“Lakini tunaamini kashata hizi haziuzwi tena na
kama zinauzwa ni kwa siri kubwa na ni vigumu kuwakamata wahusika kwa sababu
kashata ni chakula cha kawaida,”anasema.
Hata hivyo, anashauri jamii kutoa ushirikiano
katika mapambano dhidi ya biashara nzima ya dawa za kulevya, badala ya
kuwaachia askari peke yao.
‘Tunashindwa kwenye kesi zetu nyingi kwa sababu
ya kukosekana mashahidi raia; sasa ili tushinde vita hivi lazima wananchi
washiriki mapambano kwa kutoa ushahidi mahakamani kwa sababu kesi inapokosa
shahidi raia, inakosa uzito na ni rahisi mshitakiwa kuachiwa kwa sababu siku
zote mahakama inaona sisi askari tunakandamiza haki za raia,’ anasema.
“Kazi yetu ni ngumu na kama wananchi wataendelea
kuwalinda, ni vigumu kushinda kwa sababu wauzaji ni majirani zetu, wanatupa
pesa, wametuchimbia visima, hapa ndio penye ugumu wa kutajwa,”anasema.
No comments:
Post a Comment