Na Mwandishi wetu
JAMII imeaswa kuondokana na
utamaduni wa kuwapeleka mayatima katika vituo vya kulelea watoto na badala
yake kuwalea katika familia, kwani hatua
hiyo inazidisha upendo kwao.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu
wa Kitengo cha Hifadhi ya mtoto, katika Idara ya Ustawi wa Jamii, Maria Obel
Malila, wakati akitoa ufafanuzi katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi
na walezi wa vituo vya kulelea watoto nchini, yaliofanyika katika ukumbi wa
Chuo cha Mafunzo Kilimani.
Alisema wananchi walio wengi wamejenga
mazoea kuwa vituo vya kulelea watoto ndio mahala panapofaa zaidi kuwapeleka
watoto yatima, ilhali kuna watu wa karibu wa kuwalea na kuwatunza vyema.
Alisema pale mtoto anapolelewa
katika familia hupata upendo na kujengewa mazingira bora katika maisha yake ya
baadae.
“Kumpeleka mtoto kituoni iwe jambo la mwisho, pale
ambapo hakuna jinsi, ni vyema watoto wakalelewa katika familia, hupata upendo
na kujengewa mazingira bora ya maisha ya baadae,” alisema.
Aidha aliwataka baadhi ya watu
wenye hulka ya kutafuta nafasi na kuwapeleka watoto wao kulelewa katika vituo
vya kulelea watoto kwa kisingizio cha kuwa na uwezo wa duni kimaisha,
kuondokana na tabia hiyo, kwani kimsingi watoto wanaopsawa kulelewa katika
vituo hivyo ni yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu.
Katika hatua nyingine
mwezeshaji Seif Maabad, akizungumzia mahitaji ya msingi ya mpango wa malezi ya
kambo, alisema ni muhimu utafiti wa kina kufanyika kabla mlezi anaeomba mtoto, kupatiwa mtoto huyo kwa ajili ya
kwenda kuishi nae.
Alisema hatua hiyo ni muhimu,
kwa vile itaiwezezesha Idara ya ustawi wa Jamii, kufahamu iwapo walezi wanaomba mtoto hawana kumbu kumbu za makosa ya udhalilishaji
pamoja na kuwa na uwezo wa kumtunza vyema mtoto huyo.
Alisema baada ya mtoto
kupelekewa katika malezi ya kambo, kuna umuhimu wa kufuatilia maendeleo na hali
ya afya ya mtoto, elimu pamoja na ukuaji wake kisaikolojia katika jamii.
“Idara ya Ustawi wa jamii ina
jukumu la kuwakabidhi watoto kwa walezi wa kambo, lakini pia kuwaongoza watoto
katika kuangalia ustawi wao,” alisema.
Alitaka kuwepo mawasiliano ya
kutosha kati ya walezi wa mtoto na idara,
kwa kuelewa kuwa afikapo umri wa miaka 18,mtoto
hulazimu kurejeshwa alikotoka.
Mafunzo hayo ya siku tano yaliyoandaliwa
na Idara ya Ustawi wa Jamii Zanzibar na kufadhiliwa na UNICEF, yaliwashirikisha
viongozi na walezi wa vituo kadhaa vya kulelea watoto ikiwemo SOS, Islah
Centre,Saifo orphan Children,kituo cha kulelea watoto Mazizini,Fissabillillah
Fuoni, Reema Home, Montessory Orphan Organisation,Wakfu Al Mazrui na Omar Al
Khatab.
No comments:
Post a Comment