Headlines News :
KARIBU ZANZIBAR YETU BLOG, KWA HABARI MOTO MOTO KUTOKA JIKONI USIKOSE KUTUFUATILIA...ZANZIBAR MEDIA GROUP TUNAIWAKILISHA ZANZIBAR...
Home » » Sheria ya Jinai

Sheria ya Jinai

Sheria ya Jinai Namba 6 ya 2004 inashughulikia masuala yote
yanayohusu makosa ya jinai.
Makosa yaliyomo ndani ya sheria hiyo yamewekwa pamoja na kuifanya sheria hii kuwa ya kuongoza makosa ya jinai
Nini Kosa la Jinai
Kosa la jinai maana yake ni makosa yaliyomo ndani ya sheria hii.
Makosa haya yanapofanywa mtu aliyefanya kosa huwa anaadhibiwa na serikali, ingawa aliyemkosea si sirekali bali ni raia wa kawaida au chombo chenye hadhi ya kuweza kusimama kisheria.
Serikali kwa kupitia polisi hufanya upelelezi kuhusiana na tuhuma zilizoripotiwa polisi kuhusiana na makosa haya ya jinai.
Polisi inapogundua kwamba tuhuma hizo ni za kweli humshtaki Mahkamani yule aliyetuhumiwa kutenda kosa.
Kesi huendeshwa na Waendesha Mashtaka walioteuliwa na Mkurugenzi wa Mashtaka.
Mahakama nayo kwa kufuata taratibu zake husikiliza kesi kwa misingi ya kisheria na baadae humhukumu mtu aliyefanya kosa.
Hukumu inaweza kuwa ni faini, kutumikia chuo cha mafunzo, au kuitumikia jamii.
Faini hupokelewa Mahakamani, bali kutumikia chuo cha mafunzo na kuitumikia jamii husimamiwa na Idara ya Chuo cha Mafunzo.
Tofauti kati ya makosa ya jinai na ya madai
Tofauti kubwa iliyopo kati ya makosa ya jinai na madai ni kwamba katika kosa la jinai Serikali ndiyo inayoshtaki kwa niaba ya
muathirika wa tendo la jinai, wakati katika kesi ya madai mdai mwenyewe ndie anayeshtaki.
Pia adhabu katika kesi ya jinai huwa ni
kifungo, faini au kutumikia jamii, lakini katika kesi ya madai mtu huwa anadai fedha, kitu, mali au fidia ya jambo fulani.
Ufunguaji wa kesi ya jinai
Kesi ya jinai hufunguliwa na Serikali dhidi ya mtu anayetuhumiwa kutenda kosa la jinai.
 Mtu aliyeathirika na kitendo hicho au mtu aliyeshuhudia tendo hilo likitendeka ana wajibu wa kuripoti tukio hilo katika kituo cha polisi, na polisi hulishughulikia suala hilo
katika hatua zifuatazo:
(i) huchukua maelezo ya walalamikaji/mlalamikaji;
(ii) huchunguza ukweli wa lalamiko hilo;
(iii) humkamata mtu anayetuhumiwa kutenda kosa hilo; na
(iv) humpeleka Mahakamani na kumfungulia shtaka mtu huyo;
Makosa ya Jinai
Makosa ya jinai yanaweza kugaiwa katika aina mbali mbali kutegemeana na maudhui yanayozungumzwa.
Yapo makosa ya jinai ambayo mtuhumiwa anaweza kukamatwa bila ya mkamataji kuwa na hati ya kukamatia; makosa haya ni yale yanayotendeka waziwazi kama wizi, ujambazi, mauaji nk.
Pia yapo yanayohitaji hati ya kukamatia ili uweze kumkamata mtuhumiwa kwa mfano kosa la kula njama, udanganyifu, nk.
 Kwa yale makosa yasiyohitaji hati ya kukamatia hata mtu wa kawaida anaweza kumkamata mtuhumiwa
na kumuweka chini ya ulinzi, lakini anatakiwa amkabidhi haraka iwezekanavyo kwa vyombo vinavyohusika.
Vile vile makosa ya jinai yapo yanayopewa dhamana na yasiyopewa dhamana.
Makosa yasiyopewa dhamana ni kama kuua kwa makusudi, uhaini na ujambazi wa kutumia silaha.
Katika Sheria ya jinai makosa ya jinai yamegawiwa katika makundi mbali mbali.
Makundi hayo ni kama yafuatayo:
(i). Makosa yanayohusiana na uhaini au yaliyo dhidi ya Serikali ambayo yamo ndani ya Sehemu ya 7
(ii) Makosa yanayohusiana na uhusiano na nchi za kigeni ambayo yamo ndani ya sehemu ya 8
(iii). Makosa yanayohusiana na kufanya mikusanyiko isiyohalali, fujo na makosa mengine yanayohatarisha amani ambayo yamo ndani ya sehemu ya 9.
(iv). Makosa ya rushwa, utumiaji mbaya wa ofisi za umma na makosa yanayohusiana na uchumi yamo ndani ya sehemu ya 10.
(v). Makosa yanayohusiana na utoaji wa haki mahakamani, kama vile kutoa maelezo ya uongo, kupandikiza ushahidi, kuwafanya mashahidi waseme uongo, n.k. ambayo yamo
ndani ya sehemu ya 11.
(vi). Makosa yanayohusu kukimbia kutoka katika vyombo vya sheria na kuwazuia maafisa wa mahakama kufanya kazi zao ambayo yamo ndani ya sehemu ya 12;
(vii). Sehemu ya 13 imeainisha makosa mengine dhidi ya serikali kama udanganyifu, uzembe kazini, kutotii amri halali na kusababisha hasara kwa serikali;
(viii). Sehemu ya 14 inahusiana na makosa yanayokwenda kinyume na dini;
(ix). Sehemu ya 15 inahusiana na makosa ya kujamiiana.
 (x). Sehemu ya 16 inahusiana na makosa ya ndoa na majukumu ya nyumbani;
(xi). Sehemu ya 17 inahusiana na makosa dhidi ya afya ya jamii, pamoja na karaha zinazotokea katika jamii;
(xii). Sehemu ya 18, 19, 20 na 21 inahusiana na makosa ya mauaji, na yale yenye kuhatarisha maisha au afya;
(xiii). Sehemu ya 22 inahusiana na makosa yanayofanywa na vigenge vya wahalifu;
(xiv). Sehemu ya 23 inahusiana na makosa ya uzembe na dharau iliyokithiri;
(xv). Sehemu ya 24 inahusiana na makosa ya kuingilia katika mwili wa mtu mwingine;
(xvi). Sehemu ya 25 inahusiana na makosa ya utekaji nyara na uzuiaji wa uhuru wa mtu;
(xvii). Sehemu ya 26, 27, 28, 29, 30, 31 na 32 zinahusiana na makosa ya wizi, ujambazi, unyanganyi, uvunjaji wa majumba, utapeli, udanganyifu na kupokea mali za wizi;
(xviii). Sehemu ya 33 inahusiana na makosa yanayotokana na mali;
Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : Zanzibar Media Group
Copyright © 2020. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved