Headlines News :
KARIBU ZANZIBAR YETU BLOG, KWA HABARI MOTO MOTO KUTOKA JIKONI USIKOSE KUTUFUATILIA...ZANZIBAR MEDIA GROUP TUNAIWAKILISHA ZANZIBAR...
Home » » Kilimo asilia kinavyoweza kulinda mazingira, afya na uchumi

Kilimo asilia kinavyoweza kulinda mazingira, afya na uchumi

NA JUMA KHAMIS “Ya kale ni dhahabu” ni msemo maarufu unaonesha ni kiasi gani vitu vya asili vilivyo na umuhimu katika kajamii. Kwa muda mrefu wakulima wa Zanzibar walikuwa wanatumia mbolea ambayo inatoka viwanda vya nje ili kuongeza uzalishaji wa mazao katika kampeni ya kujitosheleza kwa chakula. Inawezekana kuwa kwa kiasi fulani taifa lilizalisha chakula kingi wakati wa mpango huo, lakini kwa wataaalamu wanahoji kuwa mpango huo uliangalia upande mmoja tu wa kujitosheleza chakula, bila ya kujali afya za binaadamu pamoja na mazingira, kwani kuna kiasi kikubwa cha kemikali zinazozalishwa kutoka viwanda vya Ng’ambo, ambako mbolea hizo zilitokea. Baada ya kugundua ukweli huo, sasa Zanzibar inashirikiana na wadau wa maendeleo kubadili mfumo wa kilimo unaojitenga na matumizi ya mbolea za kemikali na kushajiisha matumizi ya mbolea hai, ama mbolea asilia. Mbolea hai ni nyenzo muhimu sana kwa taifa masikini kama Zanzibar katika kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa chakula, kuimarisha uchumi wake pamoja na kuhifadhi mazingira kwa wakati mmoja. Hiki ndicho huitwa kilimo endelevu, msamiati unaowiana pia na mingine kwenye sekta ya kilimo cha kisasa, kama vile kilimo asilia ama kilimo hai. Wataalamu wa kilimo wanaeleza kuwa wakulima visiwani Zanzibar lazima wajikite katika kilimo hai, ambapo mbolea ya asili inatumika pasina kuacha madhara yoyote kimazingira wala kwa afya za binaadamu. Wataalamu wengi wanaeleza kuwa mbolea hiyo ikitumika vizuri, uzalishaji wake una faida kuwa kiuchumi na kiafya. Kilimo rafiki kwa mazingira Katika kufikia hatua hiyo ya kuwa na mbolea asilia ili kuwa na kilimo hai, Taasisi ya Fumba Town Service Center (TFTSC) kwa kushirikiana na Taasisi ya Practical Permaculture Institute (PPIZ) pamoja na Taasisi ya Milele Foundation Zanzibar (MFZ) zimeazisha mafunzo maalumu kwa vijana kupitia mradi wa ‘Fursa Kijani’ juu ya utengezaji mbolea itokanayo na vitu vya asili, kama vile vinyesi vya wanyama pamoja na mchanganyiko wa majani yaliyooza, ambapo wamewachukua vijana zaidi ya 70 kuwapatia mafunzo mbalimbali yakiwemo mafunzo ya mbolea asilia. Akizungumza na Zanzibar Leo, Mratibu wa miradi katika taasisi ya Milele Foundation Zanzibar, Bi Khadija Sharif, alieleza kuwa wameamua kufanya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) pamoja na jamii kuwashawishi wananchi kutumia mbolea asili ili kupata kilimo hai chenye mazao bora. “Ni muhimu kwa wadau wote katika jamii wafahamu faida za kimazingira na fursa za kiuchumi katika kilimo cha asili Zanzibar kwa kutumia mbolea ambazo hazina kemikali,” anaeleza Bi Khadija, akifahamisha kuwa wanawapatia vijana elimu hiyo kwa sababu wao ndio taifa la leo na hivyo ndio wanaoweza “kuleta mabadiliko na kuwa na maisha bora ambayo yatakuwa na afya kutokana uzalishaji unaotumia mbolea asilia.” Mtaritibu huyo wa Milele Foundation anasema kuwa kilimo kinachotumia mbolea za kemikali ni miongoni mwa vyanzo vya mabadiliko ya tabianchi, kwani mbolea hizo “husababisha joto jingi na ardhi kupoteza rutuba yake za asili. “Kila mwaka kiwango cha uzalishaji hupungua na mazao yake yanakuwa hayawezi kuishi kwa muda mrefu,” anasema Bi Khadija. Kaulimbiu ya ‘Kuitunza Dunia, Kutunza Watu, Mgawanyo Sawa’ Muanzilishi wa chuo cha Zanzibar Practical Permaculture Institute, Bernadette Kirsch, anaeleza kuwa kilimo endelevu na utangulizi wa njia endelevu ni muhimu katika kulinda mazingira na uhifadhi wa mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho. “Kauli mbiu yetu ni ‘kuitunza dunia, kutunza watu, mgawanyo sawa’. Tunataka kujikita katika kuleta matokeo mazuri yenye faida kiuchumi, kijamii na kimazingira,” anasema Kirsch, akionya kuwa hayo yote hayawezi kuja isipokuwa tu pale jamii itakapokubali kutumia mbolea zinazotokana na vyanzo vya asili na kuacha kutumia mbolea zilizozoeleka za viwandani. Maulidi Hemed Maulid kutoka kitengo cha Fursa Kijani katika FTSC aliiambia Zanzibar Daima kuwa wana lengo la kutayarisha mbolea ya kutosha ili waweze kuwauzia watu wengi zaidi kadiri inavyoyumkinika ili kufikia malengo ya kuwa na kilimo hai visiwani Zanzibar. “Tukiwa tunatumia mbolea hii ya asili, basi tutakuwa na kilimo kilicho bora na mazao yake yatakuwa imara na matamu zaidi, yasiyo na madhara hata kidogo kwa binaadamu,” anasema Maulidi, akiongeza kuwa kwa kushirikiana na taasisi hizo tatu, tayari wamewafundisha vijana ambao wana uwezo mkubwa. “Sasa ni kwa jamii yenyewe tu kuacha mazoea ya kutumia mbolea inayotokana na kemikali.” Miongoni mwa tafauti kubwa kati ya mbolea za viwandani zenye kemikali na mbolea asilia ni kuwa mbolea asilia haiwaangamizi wadudu waliomo mashambani hata inapowekwa kwenye mimea, bali huwachwa waendelee na maisha yao, tofauti na mbolea za kemikali, ambazo zina sumu ya kuuwa wadudu wote. “Kwa nini tusubiri tupewe ruzuku ya mbolea wakati ruzuku ipo katupatia Muumba wetu,” anasema Bi Mwatima Abdallah Juma ambaye ni Mwenyekiti wa Mradi wa Kilimo Hai Tanzania, akitoa wito kwa wakulima wa Zanzibar kurejea kwenye matumizi ya mbolea ambazo hazitumii kemikali kwa faida ya maisha yao na vizazi vyao. “Angalieni leo, unawasikia watu mara mgongo, mara miguu, huku saratani zimezidi. Yote haya ni kwa kutumia vyakula ambavyo vinatokana na mbolea zenye sumu. Wazanzibari tutumieni mbolea yetu asili ili tuokoke na mitihani hiyo,” anasema Bi Mwatima. Changamoto za kilimo endelevu Hata hivyo, hapana shaka hata kilimo endelevu cha kutumia mbolea asilia nacho kina changamoto zake. Mojawapo ni ughali sana na ulazima wakuwepo maeneo makubwa ya kilimo. “Lazima watu wajitume sana na mazao yake yatakuwa ya gharama kwa mwanzoni, lakini jamii ikielewa umuhimu wake, basi kila mmoja atalima kwa kutumia mbolea hiyo,” anasema Bi Mwatima, akieleza pia kuwa changamoto nyengine ni kuzirudisha akili za watu kuacha kilimo walichokizoea. Juma Abdallah Shikeli, ambaye ni kijana aliyepata mafunzo ya kutengeneza mbolea asilia kupitia ufadhili wa Milele Foundation Zanzibar, anasea kuwa miti ambayo inatumiwa mbolea hiyo inakuwa haraka na kumea vizuri bila ya kuathirika. Nchi nyingi duniani zimereja kwenye mfumo wa kilimo hai. Mataifa kama vile Kenya, Zimbabwe na hata Rwanda ni mifano mizuri, ingawa hadi sasa eneo linalotumiwa kwa kilimo hai ni asilimia moja tu duniani kote.
Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : Zanzibar Media Group
Copyright © 2020. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved