Home »
» Uharibifu mazingira wa msitu wa Jozani unavyoathiri Kima Punju
Uharibifu mazingira wa msitu wa Jozani unavyoathiri Kima Punju
Sera ya Taifa ya Misitu ya Zanzibar ya mwaka 1999 kifungu cha 12 kimeanisha kwamba misitu ya asili itakuwa chini ya serikali na kuratibiwa na idara itakayopewa jukumu la uzimamizi.
Lengo la sera hii ni kuhakikisha rasilimali ya misitu inalindwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa. Hata hivyo, licha ya lengo hilo, kumekuwa na uharibifu wa misitu, ukiwemo msitu wa taifa wa Jozani.
MSITU WA JOZANI
Msitu huu ambao ni urithi wa dunia, upo kilomita 35 kusini mashariki mwa Unguja, na eneo la ukubwa wa hekta 5,000. Ni makaazi ya kima punju (mbega mwekundu);mnyama anaepatikana Zanzibar pekee. Jozani umezungukwa na vijiji tisa vyenye wakaazi 42,000 ambavyo ni Pete, Kitogani, Ukongoroni, Chwaka, Charawe, Unguja Ukuu, Michamvi na Cheju.
KIMA PUNJU
Ni mnyama wa jamii ya sokwe na ndie kivutio kikuu cha utalii.
Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Mifugo, Maliasili na Uvuvi, Hamad Rashid Mohammed, watalii 50,000 wanafika msituni kuangalia kima; kila mtalii analipa dola 10 za Marekani.
Kwa kuwa hakuna sensa iliyofanywa, wataalamu wanasema idadi yao imeshuka hadi kufikia 2,000 kutokana na uharibifu unaosababisha upungufu wa chakula.
Ana manyoya ya rangi nyekundu iliyoiva na nyeusi sehemu ya mgongoni na uso wake mweusi una taji la manyoya meupe.
Alama ya rangi ya pinki midomoni na puani na mkia mrefu wenye rangi nyeusi kwa juu na nyeupe kwa chini, inamtofautisha na kima wengine.
Ni mnyama anaekunywa maji mara moja tu kwa mwaka kutokana na chakula anachokula.
Kima huishi kwenye kundi la wanyama 50-80, ambapo kila kundi lina wastani wa madume wanne na kiongozi mmoja.
Dume hulinda familia yake isiingiliwe na dume kutoka familia nyengine na inapotokea dume mwengine anataka kuongoza familia ni lazima afanye mapinduzi. Anaposhindwa hufukuzwa kundini kwa sababu ya kuasi, hivyo huishi maisha ya upweke hadi atakapofanikiwa kupindua.
Utafutaji chakula hufanywa na kundi zima. Madume hutoa mlio wa kuwaita wengine kwenda kutafuta chakula. Sauti ya dume wa kundi moja inatofautiana na kundi jengine.
Chakula chao ni majani machanga, maua na matunda mabichi. Hawali matunda mabivu kwa sababu matumbo yao hayawezi kumeng’enya sukari. Pia hula makaa wanaookota kutoka kwenye tanu zinazopigwa na wanavijiji ndani ya msitu. Mkaa huwasaidia kumeng’enya chakula na kuondoa sumu mwilini.
Kila kundi linaishi eneo lake na wanajuana kutokana na harufu, hivyo anapoingia mgeni kwenye kundi moja inakuwa rahisi kutambuliwa.
Ni mnyama wa jamii sokwe mwenye tumbo lenye chemba nne, ambalo hulitumia kuhifadhi chakula.
Msaidizi Mhifadhi Mkuu, Mzee Khamis Mohammed, anasema kima hubalehe anapofikia miaka sita. Jike husurufu kwa kutoa homoni zinazomvutia dume. Mimba hulelewa kwa miezi sita kabla ya kuzaliwa.
Anasema kwa kawaida kima huzaa mtoto mmoja, lakini anaweza kuzaa pacha. Baada ya kuzaliwa hunyonyeshwa kwa miezi 16, hata hivyo, dume huonyonya zaidi kuliko jike.
“Lengo la mama kumnyonyesha sana dume ni kumjengea uwezo wa kuja kuwa na familia yake,” anasema Mhifadhi Mkuu Msaidizi.
Kima huzaa katika mfumo wa moja kwa nne, yaaani kila kima watano; mmoja anakuwa dume.
Aidha anaishi miaka 20 hivyo katika kipindi cha uhai wake, anazaa watoto saba.
UHARIBIFU MAZINGIRA JOZANI
Hata hivyo, maisha ya kima yanahatarishwa na uharibifu mazingira katika msitu unaofanywa na wanavijiji. Uharibifu huu unasababishwa na ongezeko la shughuli za kijamii katika msitu hasa kilimo, uvunaji asali na malisho ya wanyama.
Kwa mujibu wa Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesha, uharibifu ulikuwa hekta tatu mwaka 2012 hadi hekta 141 mwaka 2015. Uharibifu huu ulitokea kati ya Oktoba na Februari kutokana na kuongezeka uvunaji asali.
Waziri Hamad asema uharibifu wa msitu unatisha na kama hatua za dharura hazitachukuliwa, kuna hatari ya kutoweka katika kipindi kifupi.
Anasema uharibifu huu unasababishwa na uchomaji moto unaofanywa na wavunaji asali na uvunaji wa magogo kwa ajili ya mkaa na mbao.
“Tuna tatizo la uharibifu wa hifadhi, kwa mara ya kwanza, tumeshuhudia maji ya bahari yakivuka barabara na kukaa kwa zaidi ya saa tatu, hili limesababishwa na ukataji mikoko,” anasema.
Aidha kwa mwaka 2016/2017, hekta 35.2 ziliharibiwa na kusababisha hasara ya shilingi 21.1 milioni.
“Hili ni jambo linalotusumbua, tunajitahidi kupanda mikoko lakini wananchi hawajaona umuhimu wake, wanaendelea kuikata kila siku,” anasema.
Mhifadhi Mkuu Msaidizi, Mzee Khamis Mohammed, anasema tatizo la uharibifu haliwezi kudhibitiwa kutokana na uchache wa rasilimali fedha na walinzi.
Anasema msitu una walinzi 16 wa kuajiriwa idadi ambayo ni ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa msitu, ambapo kila mlinzi ana eneo la zaidi ya hekta 300.
Hali hii anasema imeifanya serikali kuwatumia walinzi wa kujitolea kutoka vijiji vinavyozunguka msitu, lakini hata hivyo hawatoshi ambapo wapo sita tu.
“Hao wachache waliopo wanatishiwa maisha na kuharibiwa mazao na vyombo vyao vya usafiri, hivi karibuni mlinzi mmoja wa Cheju aliharibiwa mazao yake na mwengine pikipiki yake iliharibiwa, hali hii inawakatisha tamaa,” anasema.
Hata hivyo, anasema hao wachache waliopo hawajawahi kupatiwa mafunzo ya ulinzi na hawana silaha.
MTAZAMO WA KITAALAMU
Mtafiti Fatma Juma katika utafiti wake, ‘Forest fire in Zanzibar; a case of Jazani Chwaka Bay National Park’, anasema uharibifu wa msitu umesababisha athari kwa maliasili zilizomo ndani wakiwemo kima.
Anasema eneo kubwa la ardhi ya msitu imeharibika, hali ambayo imesababisha maji ya bahari kuvamia msitu wa juu.
“Fikiria 2015 pekee matukio manne ya uharibifu msitu yalitokea, hivyo kama hatua za haraka hazitachukuliwa, janga kubwa litatokea baadae,” anasema.
Mtaalamu wa mazingira kutoka Idara ya Mazingira Zanzibar, Dk. Aboud Jumbe, anasema kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kuulinda msitu.
Anasema, utafiti uliofanywa na Idara hiyo mwaka 2012, unaonesha asilimia 97 ya kuni zinazotumiwa kwenye bekari zinatoka misitu ya hifadhi ukiwemo Jozani.
Mkurugenzi Idara ya Misitu na Maliasili Zisizorejesheka, Ali Omar Ali, anasema kuongezeka shughuli za kiuchumi kwa wakazi wanaozunguka msitu, kunaleta tishio kwa maendeleo ya msitu.
Anasema kwa wastani, tani 40 hadi 60 za magogo zinakatwa kwa mwaka.Aidha, anasema matukio mengi ya uharibifu msitu chanzo chake ni uvunaji asali.
WANAVIJIJI
Hafidh Maulid Ali, Mjumbe wa kamati ya ulinzi wa msitu kutoka Cheju, anasema uharibifu wa msitu unafanywa kila kukicha licha ya jitihada zinazochukuliwa na serikali na asasi za kiraia.
Anasema hali hiyo imechangiwa na ongezeko la shughuli za kiuchumi hasa vikundi vya kuweka na kukopa.
“Wanavijiji wengi ni maskini na wamejiunga kwenye vikundi vya kuweka na kukopa, hali hii inawalazimisha kufanya kila njia kupata fedha ili kuchangia kikundi,” anasema.
Maryam Issa Saidi mkaazi wa kijiji cha Kitogani, ambae ni mwanachama wa vikundi vitatu vya kuweka na kukopa hana kazi ya kumuingizia kipato, hivyo hutegemea kuuza kuni ili apate pesa ya kuchangia.
UHARIBIFU MISITU DUNIANI
Utafiti wa Shirika la Kilimo na Chakula (FAO) wa 2008 kuhusu ‘matukio ya moto yanavyotofautiana,’ unaonesha ajali za moto wa misituni zimeongezeka miaka 25 iliyopita. Hata hivyo, hali ilikuwa mbaya 2002-2003 ikilingnaishwa na 1972. Chile ndio iliyoongoza kwa kurekodi matukio 57 na kuunguza hekta 35,000.
Kwa Afrika, Uganda ndio iliyorekodi matukio mengi ambapo kati ya 2004 hadi 2007, kulikuwa na matukio 20 yaliyounguza hekta 800.
SULUHISHO
Waziri Hamad Rashid anasema njia pekee ya kukabiliana na uharibifu wa msitu ni jamii kuendelea kupewa elimu juu ya umuhimu wa misitu.
Mhifadhi Mkuu Msaidizi, anasema serikali lazima ibadilishe mfumo wa ulinzi kwa kuwatumia askari wa vikosi vya serikali.
“Elimu pekee haitoshi, kama serikali inakusudia kuondoa uharibifu lazima iwatumie askari kwani wao wanaruhusiwa kutumia silaha na wana mafunzo ya ulinzi,” anasema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment