Headlines News :
KARIBU ZANZIBAR YETU BLOG, KWA HABARI MOTO MOTO KUTOKA JIKONI USIKOSE KUTUFUATILIA...ZANZIBAR MEDIA GROUP TUNAIWAKILISHA ZANZIBAR...
Home » , » Mradi wa ‘Mtoto Mwerevu’ ulete mabadiliko kwa jamii

Mradi wa ‘Mtoto Mwerevu’ ulete mabadiliko kwa jamii



NA JUMA KHAMIS
TATIZO la udumavu wa mwili na akili sambamba na upungufu wa madini ya chuma kwa watoto chini ya miaka mitano katika jamii inayoishi Kanda ya Ziwa limekuwa na athari kubwa katika katika kila nyanja kama makala haya yanavyoeleza.

Udumavu ni hali ya kutokua kwa viungo vya mtoto ukiwemo ubongo kwa kiwango kinachotakiwa kutokana na lishe duni ya mama wakati mtoto akiwa tumboni hadi anapofikisha umri wa miaka miwili. Mtoto wa aina hiyo huandamwa na magonjwa ya mara kwa mara, huwa dhaifu na mbaya zaidi maendeleo yake darasani huwa siyo mazuri.

Jamii inayoishi Kanda ya Ziwa, pamoja na kuwa karibu na Ziwa Victoria na hivyo kupata samaki lakini inaonekana wengi hawapati lishe ya kutosha, ikiwa ni pamoja na madini chuma yanayoaminika kuwa kwa wingi katika samaki hususani dagaa na mboga. Lipo pia tatizo la watu kuvua samaki au kufuga lakini wakauza kila kitu na familia yao kukosa lishe bora.

Kaya nyingi za kabila ya jamii ya Wasukuma, kwa mfano, hula ugali kila siku wakati mwingine kuanzia asubuhi, mchana na usiku bila kubadilisha au kuongezea na matunda na mboga.

Uzinduzi wa Mradi wa ‘Mtoto Mwerevu’ uliofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia shirika lake la Misaada la UK-AID kwa kushirikana na Wizara ya Afya nchini umekuja wakati mwafaka kwa mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa na matarajio ni kwamba utaleta mabadiliko chanya.

Mradi huo wa miaka mitano utahusisha mikoa mitano ya Geita, Mwanza, Shinyanga, Kagera na Kigoma na lengo lake kubwa ni kupunguza udumavu kwa watoto walio chini ya miaka mitano katika maeneo hayo. Generose Mulokozi, kiongozi wa mradi huo wa Mtoto Mwerevu anasema ana hakika watatizima lengo la kupunguza udumavu wa watoto chini ya miaka mitano katika halmashauri 36 zilizopo katika mikoa hiyo mitano.

Anasema tatizo la udumavu ambalo moja ya kiashiria chake ni urefu wa mtoto kuwa mdogo usioendana na umri wake, bado ni tatizo kubwa hapa nchini likiathiri wastani wa asilimia 34 ambayo ni zaidi ya watoto milioni 2.7 wenye umri chini ya miaka mitano. “Tatizo hili haliathiri ukuaji wa mtoto kimwili pekee bali pia kiakili,” anasema.

Mulokozi anasema sababu zilizofanya mikoa ya Kanda ya Ziwa kupelekewa mradi huo ni pamoja na kuwa na idadi kubwa ya watoto wenye udumavu ikilinganishwana wastani wa taifa uliopo. Pia anasema sababu nyingine ni viwango vya juu vya upungufu wa damu kwa akina mama na watoto sambamba na unufaikaji mdogo wa mikoa hiyo kutoka kwa wafadhili na wadau wa maendeleo hapa nchini.

Kwa nini mtoto mwerevu? Anafafanua kwamba mradi umepewa jina la ‘Mtoto Mwerevu’ kutokna na ukweli kuwa mtoto asiyekuwa na udumavu anakua vizuri kimwili, kiakili na hufanya afundishike vizuri katika masomo awapo darasani. Halikadhalika, mtoto wa aina hii anapokuwa mtu mzima, utendaji kazi wake na ufanyaji wa maamuzi huwa ni wenye ufanisi kulinganisha na aliyedumaa.

Wataalamu wanasema kwa bahati mbaya sana, mtoto akishadumaa katika siku 1,000 zinazohesabiwa tangu mimba yake kutungwa hadi anapofikisha umri wa miaka miwili, hata akija kula vizuri zaidi baadaye na kunenepa hali ya akili yake haiwezi kubadilika kutoka kwenye kudumaa.

Mulokozi anasema mradi huo utajielekeza katika kuhakikisha hizo siku 1,000 zinaeleweka na akina mama kula lishe bora pamoja na watoto wao.

Anasema mradi huo pia unajikita katika kubadili tabia za watendaji katika ngazi zote lengo likiwa ni kuzifanya halmashauri kuwa na mtazamo mpya kuhusu sababu za utapiamlo kwa watoto na hivyo kubuni, kupanga na kutekeleza mikakati mipya ya kutatua tatizo.

Anasema watoto 800,000 wanategemewa kufikiwa na mradi huo kwa kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji na kwamba mradi utasaidia kujenga uwezo watendaji wa halmashauri na sekta zote zinazohusika na masuala ya lishe katika kupanga na kufanya ufuatiliaji.

Anasema jamii inakumbushwa kuzingatia lishe na makuzi bora kwa mtoto ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mama anayejifungua ananyonyesha maziwa yake pekee kwa kipindi chote cha miezi sita ya mwanzo. Kanda ya ziwa kinara wa udumavu Naye ofisa lishe wa Mkoa wa Shinyanga, Mariamu Mwita anasema kuwa hali ya lishe katika mkoa wa Shinyanga na mingine ya Kanda ya Ziwa sio nzuri.

Anasema kwa mujibu wa takwimu zilizopo, mkoa wa Kagera ndio umekuwa kinara kwa kuwa na ailimia 41.7 ya udumavu ikifuatiwa na mkoa wa Geita wenye asilimia 40.5 Mwita anasema hali hiyo inachangiwa pia na mikoa hiyo kuwa na changamoto ya kukosa maofisa lishe wa kutosha ambao wangetoa elimu ya umuhimu wa lishe kwa jamii.

Anasema katika kipindi cha nyuma mkoa wa Shinyanga ulikuwa katika hali mbaya lakini wa sasa wamefanikiwa kupunguza tatizo hilo la udumavu kutokana na kutoa elimu ya kutosha. Jane Miller, mwakilishi kutoka katika serikali ya Uingereza anasema kuwa lishe ni suala muhimu kwa watoto na kwamba inasaidia hata kukua kwa uchumi kama watoto watakuwa na afya bora.

Joyceline Kaganda, Kaimu Mkurugenzi wa Chakula na Lishe Tanzania anasema kuwa hali ya lishe kwa hapa nchini sio nzuri na kuongeza kuwa mwaka 2015 jumla ya watoto 34 kati ya 100 walikuwa wamedumaa.

Anasema kuwa asilimia 58 ya watoto walipatikana na upungufu wa damu huku asilimia 35 wakipatikana na upungufu wa madini ya chuma huku Serikali ikilazimika kutumia shilingi bilioni 830 kama gharama katika masuala ya utapiamlo kwa kipindi hicho.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jaffo, anasema kuwa mradi huo unaweza kubadili afya za wananchi wa Kanda ya Ziwa kwa kutokomeza tatizo la udumavu kwa watoto.

Bajeti ya lishe kuongezeka Aprili 6 mwaka jana, asasi za kiraia zinazojihusisha na lishe chini ya mwavuli wa Jukwaa la Lishe Tanzania (Panita) ziliitaka serikali kutekeleza malengo ya Mkutano wa Kimataifa wa Afya (WHA), malengo ambayo Tanzania iliyaridhia.

Malengo hayo ni pamoja na kuongeza bajeti inayoelekezwa katika kuboresha hali ya lishe nchini. “Tunaitaka serikali kuongeza matumizi yake ya ndani katika kuboresha hali ya lishe kwa kuzingatia gharama zilizokadiriwa na WHA za kila mtoto Dola za Marekani 8.5 (takriban sh 18,500) ifikapo mwaka 2025,” lilisema tamko hilo.

Malengo ya WHA kwa mujibu wa asasi hizo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2025 nchi nyingi zinaondokana na utapiamlo, hususani kwa akina mama wajawazito na watoto. Tafiti kuhusu lishe zinaonesha kuna uhusiano mkubwa wa maendeleo ya nchi na lishe.

Taarifa ya kimataifa kuhusu hali ya lishe duniani (Global Nutritional Report) ya mwaka jana 2015 inaonesha kwamba nchi inapowekeza dola moja katika lishe (wastani wa sh 2,180) inategemea kupata faida ya dola 16 (sh 34,928) kutokana na uwezekaji huo.

Umuhimu wa siku 1,000 Kwa mujibu wa Panita, lishe bora katika siku 1,000 za mtoto huokoa vifo vya watoto zaidi ya 1,000,000 mbali na kuboresha afya na akili yake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba siku hizi 1,000 ndio msingi wa maisha ya binadamu yeyote.

Kiuchumi, siku hizi 1,000 kama mama atakula lishe bora wakati wote na lishe bora kwa mtoto akishazaliwa ikiwa ni pamoja na kunyonya maziwa ya mama yake pekee kwa muda wa miezi sita, huongeza uchumi wa nchi kwa maana ya kumwezesha kuzalisha pato la mwaka la (GDP) kwa asilimia 2-3.

Lishe bora pia humpunguza mtoto uwezekano wa kupata magonjwa ya muda mrefu (chronic diseases) na mzio (allergy). Lishe bora ni ipi? Kwa mujibu wa Panita, lishe ni hali ya mwili kupokea chakula chenye virutubisho vyote muhimu kwa ajili ya kuujenga, kuukinga na kuupa joto, hivyo kuuwezesha kufanya kazi vizuri.

Virutubisho hivyo ni pamoja na protini, wanga, vitamini, madini, nyuzi nyuzi na maji. Matatizo makuu ya lishe nchini yamegawanyika katika makundi matatu: Upungufu au utapiamlo wa protini na wanga; upungufu au utapiamlo wa virutubisho vya vitamini na madini na hivi karibuni kumekuwa na utapiamlo utokanao na unene kupita kiasi.

Lakini upungufu wa virutubisho vya vitamini na madini ndiyo unaoathiri zaidi sehemu kubwa ya jamii na waathirika wakubwa ni watoto walio katika umri wa chini ya miaka mitano na wanawake walio katika umri wa uzazi.

Panita inafafanua kwamba kwa kuwa mwili wa binadamu hauna uwezo wa kutengeneza virutubisho, chanzo kikuu cha virutubisho hivyo ni kutoka kwenye chakula na kwamba inatakiwa mtu, na hususani mtoto au mama mjamzito kula vyakula vinavyohitajiwa na mwili kila siku na siyo kile kinachomfurahisha kula au kinachopatikana.

Vyakula hivyo ni pamoja wanga kiasi kinachotakiwa (kama ugali, wali na maandazi), protini (nyama, maziwa, mayai na maharage) pamoja na vitamini na madini, vitu ambavyo vinapatikana zaidi kwenye matunda na mboga.
Share this article :

No comments:

Post a Comment

 
Support : Zanzibar Media Group
Copyright © 2020. Zanzibar Yetu - All Rights Reserved